Skip to main content
MTOTO AKIPATA MIMBA WAZAZI MIAKA 30 JELA SOMA HII HAPA
- WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali itatoa adhabu kali ya
kifungo cha miaka 30 jela kwa wazazi wote wawili wa mtoto wa kike
atakayekatishwa masomo na kulazimishwa kuolewa ama akipata ujauzito.
-
- Aidha amesema Serikali itamfunga jela miaka 30 kijana anayetaka kumuoa msichana anayesoma pamoja na wazazi wake.
-
- Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kumlinda mtoto wa kike
katika kuhakikisha kuwa anapata haki yake ya msingi ya kusoma kufikia
elimu ya chuo kikuu kwa kujenga mabweni na kuwachukulia hatua kali za
kisheria watu watakaowapa mimba na kuwaozesha katika umri mdogo na
kukatisha masomo yao.
-
- Majaliwa aliyasema hayo jana wilayani Hanang, mkoani Manyara katika ziara yake ya kikazi ya siku sita kwa mkoa huo.
-
- Alisisitiza kuwa kupitia sera ya kuboresha elimu nchini serikali
imeondoa michango ya fedha za kulipia bili za maji, umeme, gharama za
mlinzi na mitihani ili kumpunguzia gharama mzazi na mlezi na kuwaacha
wazazi kushughulikia maeneo mengine muhimu kwa mtoto wao.
-
- Alisema tayari kwa mwaka huu wa fedha, walimu 4,396 wa masomo ya
sayansi wameajiriwa ambapo alisisitiza kuwa wazazi na walezi wanalo
jukumu kubwa la kusimamia maendeleo ya shule ya watoto wao kwa lengo la
kupandisha ufaulu wa elimu kwa wilaya,mkoa na taifa.
-
- “Mtoto akiwa mtoro baba na mama wa mtoto huyo atashitakiwa,mtoto wa
kike asiguswe,vijana waendesha bodaboda acheni kuwalaghai watoto hao kwa
zawadi na usafiri, tutawasaka wote,” alisisitiza.
-
- Akizungumza na watumishi wa umma katika halmashauri ya wilaya hiyo,
aliwataka watumishi hao kujivunia serikali yao kwa kuienzi katika
kufanya kazi kwa nidhamu katika kuwatumikia wananchi bila kujali uwezo
wao, kabila wala rangi zao kwa kuwa wamepewa dhamana ya kusikiliza kero
zao.
-
- Majaliwa alifafanua kuwa wafanyakazi wana wajibu wa kuwatumikia
watanzania kwa kuwa wao ni waajiriwa wa serikali hivyo ni muhimu
wakatoka maofisini na kwenda vijijini kusikiliza kero na kuzitatua
badala ya wananchi kungojea viongozi wa kitaifa kuja kusikiliza kero na
malalamiko yao wakati wao ni watendaji wakuu katika maeneo yao.
-
- “Utumishi wenu hauhitaji upendeleo ama ahadi za njoo kesho, utumishi
wa awamu ya tano ni wa uwajibikaji zaidi na uwajibikaji ni pamoja na
kuwa mwaminifu katika kulinda na kusimamia kikamilifu fedha za serikali
zinazotengwa katika halmashauri husika kwa ajili ya maendeleo,” alisema.
-
- Akizungumzia soko la kimataifa la Endagaw, aliwapongeza wananchi wa
wilaya hiyo kwa kukubaliwa kujengewa soko kubwa la kimataifa ambako
wakulima watapeleka mazao yao na kuyauza lakini pia wataweza kuingiza
mapato kwa kukodisha makampuni makubwa yanayohitaji kukodi kuhifadhi
mazao kama NRFA.
-
- Aliwataka wakulima wa mazao mbalimbali wilayani Kateshi kulitumia
soko la mazao la kimataifa la Endagaw lililojengwa na ofisi yake kuuza
mazao yao kwa bei nzuri badala ya kuuza mazao majumbani ambako wamekuwa
wakiuza kwa bei ya chini isiyowasaidia kukuza kipato chao.
-
- Alieleza kuwa serikali itaendelea kjuimarisha miundombinu ya soko
hilo kwa kujenga eneo la wazi la nje kudhibiti magari makubwa
yanayoshusha na kupakia mizigo yasikwame kutokana na matope na kuwa na
mizani ya kupimia mazao na magari.
-
- Kuhusu kero ya maji katika mji wa Katesh, alisema marekebisho
yanafanyika kurekebisha mashine ya kuvuta maji na kuhakikisha sera ya
maji inatekelezwa kwa vitendo katika kumpatia maji kila mwananchi umbali
usiozidi mita 400.
-
- Awali katika taarifa yake Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Sara Msafiri
alimweleza Waziri Mkuu kuwa changamoto kubwa inayoikabili wilaya hiyo ni
migogoro ya ardhi, kuanzisha gereza la wilaya kupunguza usumbufu wa
kuwapeleka wahalifu Babati, jambo ambalo alisema atalipeleka wizara ya
mambo ya ndani lipate kushughulikiwa.
-
- Msafiri aliomba pia kujengewa mahakama ya wilaya ambapo alisema ni
mchakato uliopo wa mahakama kuu kujenga mahakama katika ngazi za wilaya
hivyo jambo hilo nalo litashughulikiwa.
-
- Mbunge wa Viti Maalum Mkoa, Ester Mahawe alibainisha tatizo la kuwa
na shule ya kidato cha tano na sita moja kwa wilaya nzima ambapo
alimwomba Waziri Mkuu kutoa kipaumbele katika bajeti zake za elimu ili
shule zaidi zijengwe mkoani humo.
-
- Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Manyara, Rose Kamili (Chadema)
aliiomba serikali kufuatilia na kuyatolea maamuzi mashamba makubwa
ambayo yamekuwa hayaendelezwi na wawekezaji kutoka Ngano Ltd
wanayoyamiliki zaidi ya ekari elfu 45 ambapo wamekuwa wakilima ekari
elfu 16 pekee na kuacha migogoro ya ardhi baina yao na wananchi na
kukosesha mapato ya halmashauri.
-
- Ziara hiyo ilipata baraka za mvua kubwa baada ya ukame wa muda mrefu
ilishangiliwa na umati wa watu waliokuwa wakiimba kwa furaha kuashiria
Waziri Mkuu kuja na baraka hiyo kuneemesha mazao yao.
-
- Leo Waziri Mkuu anatarajiwa kuhitimisha ziara yake wilayani Babati
ambapo pamoja na mambo mengine atafanya majumuisho ya ziara hiyo na
kutoa maelekezo ya serikali kwa wananchi na viongozi ngazi ya mkoa.
Comments
Post a Comment